Na. Rainer Budodi- Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene ametoa rai kwa Waajiri wote katika taasisi za umma kusoma, kuelewa na kutumia kikamilifu Mwongozo wa Ujumuishwaji wa Jinsia na kuzingatia masuala ya Jinsia katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema hayo wakati wa tukio la uzinduzi wa Mwongozo wa Ujumuishwaji wa Jinsia katika Utumishi wa Umma na Ufunguzi wa Mafunzo ya Wanawake Awamu ya Tatu na Nne yanayoendeshwa na Taasisi ya Uongozi kwa kushirikiana na Serikali ya Finland leo tarehe 16 Oktoba, 2023 katika ukumbi wa Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es salaam.
Mhe. Simbachawene ameilekeza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kusambaza mwongozo huo kwenye mamlaka zote za ajira katika Utumishi wa Umma na kushirikiana na Mamlaka hizo kuendesha mafunzo ili kuimarisha usawa na hatimaye kuondoa aina zote za ubaguzi mahali pa kazi.
“Ninawaelekeza waajiri wote katika taasisi za umma kuandaa Mpango kazi wa namna ya kutekeleza afua za usimamizi wa masuala ya jinsia mahala pa kazi na kutenga bajeti kwa kila mwaka wa fedha ili kumuwezesha Mratibu wa masuala ya Jinsia wa Taasisi husika kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na uratibu wa mafunzo ya Jinsia katika Utumishi wa Umma kwenye Taasisi husika” alisisitiza Mhe. Simbachawene.
Vilevile, amemuelekeza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI kushirikiana na Ofisi ya Rais -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuzifikia Mamlaka zote za Mikoa 26 na Mamlaka za Serikali za Mitaa 184 ili kutoa mafunzo kuhusu Mwongozo huo ili kila mtumishi wa umma apate uelewa wa kutosha na kuepuka kuwa na ubaguzi mahali pa kazi.
Vile vile, Mhe. Simbachawene amefafanua kuwa ili Taifa liweze kufikia usawa wa kijinsia, hasa kwenye masuala ya uongozi, hakuna budi kushirikisha wanaume katika utekelezaji wa mipango na jitihada mbalimbali za kufanikisha azma za wanawake kuwa viongozi.