Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Bi. Neli Msuya amesema huduma ya majisafi inaendelea kuimarika kadri miradi iliyopangwa na Serikali inavyoendelea kukamilka.
Amesema hayo wakati wa mapokezi ya shehena ya mabomba ya ukubwa wa inchi 12 kwa ajili ya kuendeleza mtandao wa usambazaji maji kwa umbali wa kilomita 6.9 kutoka eneo la Buswelu hadi Ilalila, Wilayani Ilemela.
"Niwasihi wananchi waendee kushirikiana nasi MWAUWASA; miradi ya kuboresha huduma ya maji inaendelea kutekelezwa maeneo mbalimbali na kadri inavyokamilika ndipo huduma nayo inaendelea kuimarika na si suala la siku moja; maendeleo ni hatua," Bi. Neli amesema.
Ameongeza kwa sasa MWAUWASA itafungua Madawati ya Huduma kwa Wateja kwa ajili ya kurahisisha ushirikishwaji na mawasiliano kwa wananchi, kufikisha elimu na kutoa taarifa za hatua mbalimbali za ujenzi wa miradi kwa kushirikiana na viongozi wa maeneo husika.
"Tunashukuru viongozi na wananchi kwa ujumla kwa ushirikiano wanaoendelea kutupatia wakati huu tukitekeleza miradi; niwasihi tu msichoke kila tunapowaita ili kuwapa mrejesho," Bi. Neli amesema.
Amesisitiza kuwa miradi hiyo inafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia mia moja ikiwa ni jitihada za Rais. Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.
Amesema mradi wenye thamani ya shilingi bilioni 4.7 utafikisha huduma ya maji kwenye maeneo ambayo hayakuwa na mtandao toshelevu hapo awali na pia kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwenye maeneo yaliyo na changamoto.
Utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 53 na mtandao wa bomba umbali wa kilomita 14 umelazwa na matarajio ni kukamilisha mradi ifikapo Desemba 15.
"Tunafanya kazi kwa kasi ili Desemba 15 tuwe tumekamilisha mradi hasa ikizingatiwa kwamba tunaelekea kwenye msimu wa mvua nasi hatutaki kuwa na kikwazo kwani fedha tayari tunayo, nguvu kazi ipo ya kutosha na tunashirikiana kwa karibu na viongozi wa maeneo husika na jamii," Bi. Neli amesema.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Shibula, Mhe. Swila Dede ameishukuru Serikali kwa niaba ya wananchi kwa mradi wa maji.