Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Afya Dkt.Wilson Mahera amewataka watoa huduma za afya nchini kutoa huduma bora za afya,ustawi wa jamii na lishe ili kuendana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali.
Dkt.Mahera ameyasema hayo Oktoba 5, 2023 kwenye kongamano la afya linalofanyika jijini Dar es salaam.
Amesema kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya hivyo uwekezaji huo uendane na huduma bora kwa wananchi.
“Serikali imeendelea kufanya uwekezaji wa miundombinu,vifaa tiba na rasilimali watu, tumeajiri watoa huduma na tunawajengea uwezo wafanyakazi wetu kwa kuwapa mafunzo mbalimbali na kuboresha maslahi yao,haya yote tunayafanya ili nanyi msiwe na sababu ya kutotoa huduma nzuri kwa jamii mnayoihudumia,” amesema.
Aidha, amesema serikali inaandaa mkataba wa ufanisi kati ya serikali na watoa huduma za afya ili kupima utendaji wao katika kutoa huduma na wale watakaofanya vizuri watapewa motisha na watakaofanya vibaya watachukuliwa hatua.
Kongamano la afya Tanzania limehitimishwa leo kwa wizara ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kuwasilisha mada mbalimbali zinazohusu Idara ya Afya Ustawi wa jamii na Lishe huku wizara ikipokea Tuzo ya utekelezaji bora wa huduma za afya ya msingi nchini.