Na. WAF - Dar es Salaam.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema takwimu za Wizara ya Afya kupitia MTUHA (DHIS -2) zinaonesha kumekuwa na ongezeko la asilimia 9.4 kwa magonjwa ya Moyo na Shinikizo la Juu la Damu pekee kutoka wagonjwa Mil. 2.5 Mwaka 2017 hadi wagonjwa Mil. 3.4 Mwaka 2022.
Waziri Ummy ameyasema hayo leo Septemba 29, 2023 kwenye maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam.
“Takwimu za Wizara ya Afya kupitia MTUHA (DHIS-2) zinaonesha kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa Moyo na Shinikizo la Damu kwa asilimia 9.4”. Amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy amesema taarifa za ufuatiliaji wa magonjwa yasiyoambukiza kutoka mwaka 1980 hadi mwaka 2020 inaonesha ongezeko la magonjwa ya Shinikizo la juu la Damu na Kisukari katika jamii kutoka asilimia 1 hadi 9 kwa wagonjwa wa kisukari na kutoka asilimia 5 hadi 26 kwa wagonjwa wa Shinikizo la juu la Damu.
“Magonjwa haya mawili ndiyo chanzo kikuu cha magonjwa ya Moyo, Figo pamoja na ugonjwa wa Kiharusi hivyo ongezeko hili ni tishio kwa ustawi wa Afya ya jamii yetu na ndiyo sababu inatuweka hapa leo kujadili mikakati ya kukabiliana nayo”. Amesema Waziri UmmyAidha Waziri Ummy amesema, Magonjwa ya Moyo na ugonjwa wa Kiharusi yanaweza kuzuilika kwa mtu mmoja mmoja na jamii yetu kwa kuweza kuchukuwa hatua za haraka.
Hata hivyo, Waziri Ummy amesema idadi ya watu wazima wanaofanya mazoezi ni imeongezeka ukilinganisha na vijana huku akiwasihi kutenga muda Zaidi wa kufanya mazoezi
Pia, Waziri Ummy amesema kupunguza matumizi yaliyokithiri ya chumvi, sukari na mafuta ya kupikia kwa kuzingatia ushauri wa muhimu unaotolewa na madaktari kwa kufanya hivi kutaweza kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo tatizo la Moyo.