DKT. MSONDE AWAPA SOMO WALIMU KUONGEZA UMAHIRI WA LUGHA YA KINGEREZA SEKONDARI

MUUNGANO   MEDIA
0

Angela Msimbira, Mpwapwa.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dkt. Charles Msonde amewataka walimu kuongeza umahiri wa kuongea na kuandika lugha ya kingereza kwa wanafunzi wa sekondari.


Akifungua mafunzo  kwa wakuu wa shule za Sekondari kuhusu  ufundishaji wa awali wa Kingereza  kwa wanafunzi  wanaomaliza  darasa la saba kwa Mkoa wa Dodoma yaliyofanyika  Chuo Cha Ualimu Mpwapwa, Dkt.Msonde amesema ni vyema

kubainisha tatizo na kutafuta njia mbadala ya kuwawezesha watoto kujua lugha ya kingereza.

Amesema mwalimu anawajibu wa kufundisha wanafunzi umahiri wa kuandika na kuongea kingereza.


"Mahali popote penye changamoto lazima itatuliwe ila kinachotakiwa ni kutambua nguvu na shida ipo wapi hivyo ukiweza kuipata changamoto na kuweza kuitatua unaleta mabadiliko,"amesema.


Amewapongeza  viongozi wa Mkoa wa Dodoma  kwa kuamua kwa dhati  kushirikisha Halmashauri zao kwa kuhakikisha wanatafakari kwa kina changamoto zinazoikabili sekta ya elimu nchini hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali ina mkakati wa kuboresha elimu nchini.


"Serikali imeamua kuleta mabadiliko katika English Orientation Course kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi waliomaliza darasa la saba wanajua kuandika, kusoma na kuongea kingereza lengo ni mwalimu aweze kueleweka pale anapofundisha darasani,"amesema.

Amesema kuwa lugha ndio msingi wa kila kitu na hasa kwa shule za sekondari hivyo amewataka wakuu wa shule kuhakikisha wanatatua changamoto hiyo shuleni.


“Katika kuhakikisha unatatua changamoto wa kitu fulani lazima utambue nguvu ya adui hivyo tunapotaka kuboresha elimu ya sekondari tutambue changamoto kubwa ya wanafunzi wa sekondari ni umahiri wa lugha ya kingereza hivyo ni vyema kubainisha tatizo na kutafuta njia mbadala ya kuwawezesha watoto kujua lugha ya kiingereza"amesema.


Naye, Afisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma, Gift Kyando amesema dhamana ya elimu kwa upande wa shule za sekondari ipo mikononi kwa walimu wakuu wa shule hivyo wanawajibu wa kuwafundisha watoto umahiri wa kujua na kutambua  lugha ya kingereza nchini.


Amesema kuwa Mkoa wa Dodoma inatarajia kuanza Orientation kwa kidato cha kwanza kuanzia Oktoba 9, 2023 hivyo imeamua kuwajengea uwezo walimu ili waweze kutimiza lengo la Mkoa la kuleta mabadiliko  katika sekta ya elimu

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)