Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko akizungumza na
wananchi katika Kijiji cha Ihako wilayani Bukombe Mkoa wa Geita mara
baada ya kuwasha umeme katika Kijiji hicho tarehe 26 Septemba, 2023.
Moja ya nyumba iliyounganishwa na umeme katika Kijiji cha Ihako
wilayani Bukombe mkoani Geita.
DKT. BITEKO APELEKA SHANGWE ZA UMEME KIJIJI CHA IHAKO, BUKOMBE
AIAGIZA REA KUELEKEA VIJIJINI
Teresia Mhagama na Godfrey Lulinga
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameanza
kazi ya kuwasha umeme vijijini ambapo leo amewasha umeme katika
Kijiji cha Ihako, wilayani Bukombe mkoani Geita na hivyo kuwezesha
wananchi katika kijiji hicho kuanza kutumia rasmi nishati hiyo.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho, Dkt. Biteko amepongeza
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kazi nzuri ya kupeleka umeme
vijijini ikiwemo kijiji cha Ihako na kuelekeza kuwa, sasa mwendo ni
wa mchakamchaka kupeleka umeme kwa wananchi wote waliopo vijijini.
"REA nendeni vijijini, muda wa kufanya vikao kwenye maukumbi makubwa,
au makao makuu ya miji hatutaki, tunataka tuwaone mnaenda vijijini
kupeleka umeme, nyie ni Wakala wa Nishati Vijijini siyo Wakala wa
umeme mijini , vikao vyenu viwe na wananchi na magari yenu yapite humo
wanamopita wananchi wenye maisha ya kawaida kabisa, " amesisitiza Dkt.
Biteko
Ameongeza kuwa, Serikali inataka kuona shuguli za kupeleka na kuwasha
umeme vijijini zinatokea, na kwamba umeme huo uingie kwenye nyumba
zote bila kubagua kwani kila mwananchi anahitaji umeme.
Aidha ameelekeza kuwa, mahali penye changamoto za umeme zitatuliwe
kwa haraka na si kumsubiri, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kutatua
changamoto wakati wa ziara zake wakati wasaidizi wake wapo.
Amesema kuwa fedha za kupeleka umeme vijijini zipo ambazo
zimechangiwa na wananchi, Serikali na wadau wa maendeleo hivyo hakuna
sababu ya kukwamisha miradi ya umeme nchini.
Kuhusu nishati safi ya kupikia, amesema kuwa, Serikali inataka ione
wananchi wanatumia nishati hiyo na kwamba REA waweke mpango ili
mitungi ya gesi iwafikie wananchi wa kawaida nchini na hivyo
kuwaondolea matumizi ya nishati ambayo si salama.
Vilevile amesema kuwa, Serikali inafanya jitihada mbalimbali ili
kupata umeme wa kutosha kutoka vyanzo vya umeme ikiwemo Mradi wa
Julius Nyerere ( MW 2115) ambao utaongeza kiasi kikubwa cha umeme
kwenye gridi ya Taifa na hivyo wadau wa umeme watapata umeme wa
kutosha ikiwemo viwanda, wachimbaji wadogo na wenye shughuli
mbalimbali za kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy,
amesema kuwa, Mkoa wa Geita una jumla ya Vijiji 461 ambapo vijiji 399
sawa na asilimia 86.6 vimepata huduma ya umeme kupitia miradi ya REA
Awamu ya Tatu mzunguko kwanza, REA Awamu ya Pili na REA Awamu ya
Kwanza.
Amesema kuwa, REA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali mkoani Geita
ambapo wakandarasi wapo maeneo ya miradi wanaendelea na kazi na
kuitaja miradi inayoendelea kuwa ni REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa
Pili, mradi wa kupeleka umeme pembezoni mwa miji Awamu ya Tatu , mradi
wa kupeleka umeme kwenye migodi midogo na maeneo ya kilimo pamoja na
mradi wa kupeleka umeme kwenye vituo vya afya na pampu za maji.