WAHASIBU TUME YA MADINI WAPONGEZWA KWA UTENDAJI KAZI.

MUUNGANO   MEDIA
0




Watakiwa kuongeza ubunifu na kuhakikisha Sekta ya Madini inazidi kupaa.

Wahasibu wa Tume ya Madini wamepongezwa kwa mchango mkubwa kwenye utendaji wa Tume ya Madini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Tume inapata hati safi na kutakiwa kuongeza  ubunifu kwenye utendaji kazi ili mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa uendelee kuongezeka na kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.

 

Hayo yamesemwa leo  na Mkurugenzi wa Huduma za Tume ya Madini, CPA William Mtinya jijini Dodoma kupitia mahojiano maalum mara baada ya  kufungua kikao kazi cha siku tatu kwa wahasibu wa Tume kwa ajili ya matumizi ya mfumo mpya wa manunuzi Serikalini (National e-Procurement System of Tanzania) na uwekaji wa kumbukumbu sawa kwa ajili ya ukaguzi wa hesabu kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba.

 

Amesema kuwa ili kuhakikisha malengo ya Tume ya Madini yanafikiwa hususan kwenye makusanyo ya maduhuli ni vyema wahasibu wakahakikisha wanafanya kazi kwa ubunifu na kuwa washauri wakuu wa viongozi wao wakiwemo Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa huku wakihakikisha taratibu zote za malipo ikiwa ni pamoja na manunuzi zinafuatwa.


Katika hatua nyingine, CPA William Mtinya amesema kuwa Serikali kupitia Tume ya Madini imejipanga katika kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kukua ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma kwenye Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, Masoko ya Madini na Vituo vya Ununuzi wa Madini vilivyoanzishwa.


 

Ameongeza kuwa, Tume ya Madini inaendelea kutoa elimu kuhusu ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini mikoani kupitia semina na vipindi vya redio na televisheni ili kuhakikisha watanzania wengi wananufaika na rasilimali za madini kupitia utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini kama vile ajira, vyakula, ulinzi pamoja na kufungamanisha na Sekta nyingine muhimu za kiuchumi.


Ameendelea kusema kuwa pia elimu kuhusu usalama wa afya na mazingira kwenye shughuli za uchimbaji wa madini imeendelea kutolewa lengo likiwa ni kuhakikisha wachimbaji wa madini wanaendesha shughuli zao bila kuathiri mazingira na afya za wananchi wanaozunguka migodi yao.

 

Awali akielezea manufaa ya matumizi ya mfumo mpya wa  manununuzi, Mkurugenzi wa Manunuzi wa Tume ya Madini, Chenduta Makawa amesema kuwa mfumo utaongeza uwazi kwenye manunuzi ya umma sambamba na kurahisisha utoaji wa huduma ndani ya muda mfupi.



Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)