Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Jumanne Sagini amekea vikali tabia ya vijana kujihusisha na vitendo vya ubakaji kwa wanafunzi wa kike na kusisitiza kuwa kwa wale wote watakaobainika maeneo ya kuwahifadhi ili kuwafundisha adabu yapo ya kutosha.
Naibu Waziri Sagini ameyasema hayo wakati wa ziara yake katika Jimbo la Ushetu Wilaya ya Kahama wakati akikagua shughuli za ujenzi wa Kituo cha Polisi Ushetu na kukagua kituo kinachotumika sasa cha Nyamilangano.
Awali akisoma taarifa ya matukio ya uhalifu katika jimbo hilo la Ushetu Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Ushetu SSP Chrisantus Kavishe amesema kuwa Mahabusu waliopo kituoni hapo tisa wanatuhumiwa kwa kesi za ubakaji wa Wanafunzi wa kike na kesi kumi na nne kwa kusababisha mimba kwa Wanafunzi.
Akizungumza katika Mkutano wa hadhara na Wananchi wa Kijiji cha Nyamilangano mara baada ya ukaguzi huo Naibu Waziri Sagini amewataka wazazi kuendelea kutoa elimu ya malezi kwa watoto wao wa kiume na wa kike na kuwasisitizia watoto wa kike kuzingatia elimu badala ya kujihusisha na masuala ya mapenzi jambo ambalo linapoteza mwelekeo wa maisha yao.