NCHI ZA AFRIKA ZATAKIWA KUUNGANA KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA.

MUUNGANO   MEDIA
0

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezitaka Nchi za Afrika kuendelea kuungana pamoja katika mapambano dhidi ya Rushwa Barani Afrika.


Rais Dkt. Mwinyi ameeleza hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika Hafla ya ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya mapambano dhidi ya rushwa Barani Afrika iliyofanyika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).


Amesema ushirikiano wa Nchi hizo kutapunguza tatizo la rushwa kwa kiwango kikubwa katika jamii na Nchi za Afrika hatua ambayo itaongeza utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa haki pamoja na kuongeza kasi ya maendeleo.

 

Rais Dkt. Mwinyi amesema rushwa ni adui wa haki pia ni kikwazo kikubwa cha maendeleo katika sekta zote hivyo ni wajibu wa kila mwananchi, Taasisi binafsi na za Umma na asasi za kiraia kuwa mstari wa mbele kupambana na adui huyo mkubwa. 

Aidha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameeleza kufurahishwa kwake kuona maadhimisho hayo yanakwenda sambamba na maonesho maalum ambapo amewataka watanzania na wageni wa Mkutano huo kutoa maoni yao juu ya namna bora na rafiki ya kupambana na rushwa Nchini Tanzania na Barani Afrika kwa ujumla.


Pamoja na hayo ameeleza kuwa Tanzania ni moja wapo wa nchi zilizosaini na kuridhia mkataba wa umoja wa Afrika wa kuzuia na kupambana na rushwa uliosainiwa na wakuu wa Nchi wanachama wa Umoja Afrika Jijini Maputo Nchini Msumbiji.


Mhe. Rais Dkt. Hussein Mwinyi Ameushukuru Uongozi wa Bodi ya Ushauri wa masuala ya rushwa ya Umoja wa Afrika kwa kuichagua Tanzania kuwa ni mwenyeji wa Maadhimisho hayo na kuahidi kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar anayoiongoza yeye zitaendelea kupambana dhidi ya rushwa kwa bidii.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejmemti ya utumishi na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene ameeleza kuwa Maadhimisho hayo yamejumuisha wadau, Taasisi na Mamlaka zinazopambana rushwa Afrika ambapo wataweza kukaa na kujadiliana pamoja kujua namna ya kuendeleza kupambana na rushwa Barani Afrika.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)