MTUMISHI WA AFYA KITUO CHA KIVULE, ALIYEKIUKA MAADILI YA KITAALUMA ASIMAMISHWA KAZI.

MUUNGANO   MEDIA
0

Na. WAF, Bariadi -Simiyu.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amepongeza hatua iliyochukuliwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kwa kumsimamisha kazi mtumishi wa afya katika Kituo cha Afya Kuvule kufuatia kuonekana kwenye video akiwa akisafisha vyombo vya Hospitalini kwa njia isiyofaa.


Waziri Ummy amesema hayo leo akiwa Bariadi, Simiyu kwenye ziara yake ya kukagua ubora wa huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya ambapo amebainisha kuwa kitendo alichofanya mtumishi huyo hakikubaliki hata kidogo.


“Tumeona juzi kule Dar Es Salaam, mtumishi anaosha vyombo vya Hospitali kwa maji ya baridi na kuanika juani, sijawahi kuona na nimefurahi kuona kuna hatua imechukuliwa, hivi ni kweli mtumishi unafundishwa hivyo kuosha vyombo na kuanika juani? amesema Waziri Ummy Mwalimu.


Kufuatia kusambaa kwa video ya mtumishi huyo akisafisha vifaa vya Hospitalini kwa njia isiyo rasmi, mnamo Julai 8, 2023 Waziri Ummy Mwalimu alitoa tamko na kusema kuwa Mtumishi huyo alikuwa amefanya kosa kwa kukiuka Miongozo ya Kanuni za Udhibiti wa Maambukizi wa Magonjwa (Infection Prevention and Control)

Aidha Mhe. Ummy amewasisitiza watumishi wa Afya kuzingatia weledi katika Majukumu yao ya kazi, huku akiwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwachukulia hatua za kisheria watumishi wanakiuka maadili na miiko ya kazi zao.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)