Na Mwandishi Wetu
Katika hali kuendelea kumtia moyo, Mariam Mwakabungu (25) anayejitolea kukumbatia watoto njiti waliotelekezwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Amana, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis amemtembelea na kumpatia kiasi cha Sh. Milioni 1.
Mwanaidi amemtembelea Mariam ikiwa ni siku chache tangu Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuweza kumpongeza na kupatia kiasi cha Sh. Milioni 2.
Akizungumza mara baada ya kumtembelea kwenye wodi ya watoto njiti iliyopo katika Hospitali hiyo, Mhe. Mwanaidi amesema kuwa lengo la kufika katika Hospitali hiyo ni kumpongeza pamoja na kumtia moyo ili kuhakikisha anakuwa na amani katika malezi ya watoto hao.
"Tumekuja katika Hospitali hii ya Amana kumsaidia huyu mama pamoja na kumpongeza na sisi kama Wizara tunaungana na Rais wetu Samia Suluhu Hassan kuhakikisha mama huyu anaishi vizuri. Lakini pia kuhamasisha kina mama wengine nao watakaposikia jambo kama hili waweze kuja kuwasaidia watoto hawa.
"Hata hivyo niwaombe maofisa wetu wa Ustawi wawe wanapita kila Zahanati kuhakikisha wanaibua changamoto zilizopo na kuzileta katika Wizara ili iweze kuzifayia kazi kwa haraka," amesema na kuongeza:
"Nitoe tu wito panapotokea changamoto tusiwe kimya tuziibue ili ziweze kushughulikiwe na serikali kwani ipo tayari" amesema Mhe. Mwanaidi.
Mwanaidi ametumia fursa hiyo kumpongeza Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kwa kufanikisha kumpatia ajira ya mkataba.
Naye Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Amana, Dk. Bryceson Kiwelu amesema jambo hilo liligunduliwa na wauguzi wa kitengo hicho kwa kushirikiana na madaktari wao.
"Walitushirikisha tukaona ni jambo jema sana. Tunaona fahari na tuko tayari kubuni mambo mengine zaidi.
"Hospital imekuwa ikifanya kazi na makundi mbalimbali ya kijamii, sio tu huyu mama ameibuliwa wapo wengi ambao walikuja kama wafanya usafi na tumeona jinsi ambavyo walifanya vizuri na kupata fursa," ameeleza Dk. Kiwelu.
Amebainisha kuwa tayari Mariam ameshaweza kuwasaidia watoto watatu ambapo wawili wanaendelea vizuri na wamepelekwa katika vituo vya kulelea watoto yatima.