HUDUMA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA SIMIYU ZINARIDHISHA - WAZIRI UMMY.

MUUNGANO   MEDIA
0

 

Na. WAF - Bariadi, Simiyu.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameridhiswa na huduma zinazotolewa katika hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu zikiwemo huduma za ICU, huduma za uzazi mama na mtoto pamoja na huduma za Radiolojia (X-Ray). 


Waziri Ummy ameipongeza hospital hiyo kwakuwa ni hospitali mpya ambapo imeanza na miundimbinu michache lakini imeweza kuonesha mfano mzuri katika utoaji wa huduma bora. 


“Hospital hii ni hospitali changa, hospitali mpya ambapo imeanza na miundombinu michache lakini mmeonesha umuhimu wa kujitoa kwa kuweza kusaidia kutoa huduma bora ukilinganisha na hospitali nyingine”. Amesema Waziri Ummy


Aidha, Waziri Ummy amesema upatikanaji wa dawa katika hospitali hiyo ni asilimia 90, upatikanaji wa vipimo na kuwataka wafamasia kuendelea vizuri katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa kwakuwa ndio dhamira ya Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

“Tunajua wengine tunamiliki maduka ya dawa lakini tunataka mtu akija hapa tunataka mtu atoke hapa akiwa amepata huduma zote ikiwemo dawa na vipimo vyote”. Amesema Waziri Ummy


Lakini pia, Waziri Ummy amewataka wataalamu hao wa Afya kuimarisha udhibiti wa dawa na vitendanishi pamoja na kuacha kumwandikia mtu dawa ambazo hazipo kwenye mwongozo wa Standard treatment guidline (STG).


Amesema, Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuchukua hatua mahususi za kuboresha huduma katika hospitali zetu hasa katika hospitali za Rufaa za Mikoa ambapo amefanya maamuzi ya kuacha fedha za makusanyo katika Mkoa huo kiasi cha Tsh: Bil. 1 na Mil. 300 ziendelee kubakia ili kuboresha huduma za afya. 


“Katika kuendelea kuboresha huduma za Afya nchini Rais Samia amefanya maamuzi mazuri ambayo ni magumu juu ya makusanyo yote ya Tsh: Bil. 1 na Mil. 300 kubakia katika Mkoa wa Simiyu ili kuzitumia kwa kuboresha huduma na kulipana stahiki pamoja na posho kwa wakati”. Amesema Waziri Ummy

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Nawanda amesema Serikali imepeleka zaidi ya Bil. 21 katika Mkoa huo ambazo zimetekeleza miradi zaidi ya 117 kuanzia katika hospitali ya Rufaa hadi ngazi ya Zahanati.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)