Akizungumza katika Bonanza maalumu lililoandaliwa na Chama cha Maafisa Usafirishaji ( Bodaboda) katika Wilaya ya Butiama Mwenyekiti wa Waendesha Bodaboda Samson Samwel Atoo amesema kuwa lengo la Bonanza hilo ni kuwaunganisha kwa pamoja, kupiga vita na kukemea matukio ya kihalifu yakiwemo mauaji yaliyotokea mwezi uliopita ambapo waendesha bodaboda 03 walipoteza maisha kwa kushambuliwa na kuuawa kinyama.
Kwa upande wake Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo na Butiama Mhe. Jumanne Sagini amesema kuwa wale wote waliokuwa wanajihusisha na mauaji yale wamekamatwa na uchunguzi unaendelea kufanyika ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
"Nataka niwaambie Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan haitaki kumpoteza kijana hata mmoja au Mwananchi yoyote yule kwa sababu ama za ujambazi au udereva mbovu barabarani au migogoro baina ya wakulima na wafugaji.Ni aibu kuwa na matukio ya uhalifu tutawakamata wahalifu wote.Niwaombe vijana tuache kutumia njia za mkato kujipatia fedha."Alisema Sagini
Katika hatua nyingine Sagini amesema kuwa Jeshi la Polisi lipo imara na linawataalamu wenye ujuzi wa kutosha kuwabaini watu mbalimbali wanaojihusisha na matukio ya kihalifu na hivyo amewaasa wale wote wanaotamani kushiriki kufanya uhalifu kuacha mara moja.
Sagini amesema kuwa Serikali inaunga mkono jitihada za bodaboda hao katika kukemea na kupinga matukio ya kikatili na mauaji ni jambo jema na Serikali haitamani kusikia kuendelea kwa matukio hayo.
Tamasha hilo lilihusisha michezo mbalimbali ikiwemo.mpira wa miguu,kuvuta kamba, kukimbiza kuku, riadha na washindi waliibuka na zawadi mbalimbali zikiwemo fedha taslimu na mbuzi.




