SERIKALI YAAHIDI UTENGENEZAJI KIWANJA CHA MICHEZO HAI KILIMANJARO.

MUUNGANO   MEDIA
0

SERIKALI kupitia Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo imeahidi kutoa kipaumbele suala la kutengeneza kiwanja cha michezo cha Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro kilichopo eneo la Half London Bomang’ombe kwa lengo la kuinua vipaji vya vijana na hivyo kutoa fursa ili vijana wanufaike kupitia Michezo na Sanaa.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na michezo Mhe. Hamisi Mwinjuma (Mwana FA) wakati akikabidhi zawadi mbalimbali kwa vijana Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro mara baada ya kumalizika kwa michuano ya Saasisha Cup iliyokuwa ikifanyika kwa mwezi mmoja na kuhusisha timu mbalimbali za soka za wilaya hiyo.

Aidha Katika fainali hiyo timu ya Machame City Fc ilishuka dimbani ikichuana na Mailisita Fc ambapo Mailisita Fc iliibuka na ushindi wa magoli 2-0 hivyo Kupata tiketi ya kujizolea zawadi mbalimbali zikiwemo jozi mbili za jezi, mpira, fedha taslimu shilingi 500,000, kombe la ushindi na medali.

Awali akizubgumza katika zoezi hilo Mbunge wa Jimbo la Hai Mhe. Saasisha Mafuwe alisema dhamira yake ya kutaka kuibua vipaji vya vijana hao huku matamanio yake yakiwa ni kuwaona wakicheza katika klabu kubwa za mpira wa miguu hapa nchini kama vile Simba na Yanga pamoja na kuwaondoa kuwa tegemezi kwa kusubiri kuajiriwa maofisini.

Sanjari na hayo baada ya kumalizika kwa mashindano hayo Naibu waziri aliketi na kuzungumza na jukwaa la wasanii wilaya ya Hai ambapo walipata fursa ya kueleza changamoto zao na kumuomba Naibu Waziri huyo ambaye pia ameyaishi maisha ya Sanaa, kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Hai Wang’uba Maganda amempongeza mbunge huyo kwa kuanzisha mashindano hayo na kumwomba kufikiria tena kuanzisha michuano mingine ili vijana waliokosa fursa hiyo awali nao waipate.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)