Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema kuwa serikali itaendelea kulinda uhuru wa vyombo vya habari na kuhakikisha vinastawi.
Amesema lengo la serikali ni kuona sekta ya habari na vyombo vya habari vinakuwa imara na vinatekeleza majukumu yake inavyotakiwa.
Msigwa ameyasema hayo leo Aprili 19,2023 Jijini Dodoma wakati akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali ambayo iliambatana na futari.
Aidha ameongeza kuwa kuelekea siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kitaifa itakayofanyika Zanzibar kuanzia Mei 01 hadi 03,2023 wanatarijiwa kuwa na wadau wa habari kujadili mstakabali wa vyombo vya habari, uhuru wa vyombo hivyo, hali za Waandishi wa Habari, Usalama wa Waandishi hao na masuala ya sayansi na teknolojia.
"Chapeni kazi kwa kuzingatia sheria penye changamoto tushirikishane ili tuweze kuzitatua na jueni tu serikali inatambua sana kazi zenu,"amesema Msigwa.
Sanjari na hayo amesema serikali ipo kazini na hakuna mradi wowote uliosimama au utakaosimama kwa sababu yoyote ile hivyo miradi ya maendeleo inazidi kuchanja mbuga.
Akiongelea kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) Msigwa amesema kuwa, ripoti imetolewa lakini haizuii kazi za Serikali kuendelea hasa katika miradi ya kimkakati ambapo wameagiza mabehewa 59 na yaliyo tayari ni 14, yaliyokuja ni 45 na maandalizi yake yamekamilika kwa 93% hivyo wakati wowote yatafika nchini.
Amesema ripoti hiyo ni moja ya nyenzo ambazo Serikali inazitumia katika kusimamia rasilimali za Watanzania, pia inatumika katika kuangalia ni maeneo gani yanahitaji kuongezewa nguvu katika usimamizi wa rasilimali za Watanzania na hatua gani zinapaswa kuchukuliwa ili rasilimali hizo ziendelee kuwa salama.


