Na.Elimu ya Afya kwa Umma.
Wizara ya Afya,Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani(UNICEF) kupitia Mtandao wa Kidini unaoundwa na taasisi nne za kidini -Tanzania Interfaith Partnership(TIP) imetoa mafunzo ya Mapambano ya Ugonjwa wa Marburg kwa Madiwani 60 kutoka kata za Halmashauri ya Wilaya Bukoba pamoja na Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.
Kati yao, madiwani 41 ni kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba na madiwani 19 ni kutoka Manispaa ya Bukoba ikijumuisha katibu wa Mbunge, Mstahiki Meya wa Manispaa,Mwenyekiti wa Halmashauri ,Madiwani wa Kata pamoja na Madiwani wa Viti Maalum.
Katika Mafunzo hayo madiwani wametakiwa kuwa mabalozi katika suala la uelimishaji juu ya ugonjwa wa Marburg ikiwa ni pamoja na kuendelea kuhamasisha jamii kuendelea kuwa na desturi ya kunawa mikono mara kwa mara pamoja na utoaji wa taarifa mapema pindi mtu anapobainika kuwa na dalili za ugonjwa huo.
“Kazi kubwa ni kuhakikisha mikono inakuwa salama ,madiwani kuweka nguvu panakuwa na miundombinu ya kunawa mikono ,ninyi viongozi ni sehemu kubwa katika kufikisha ujumbe ,ni muhimu kutoa taarifa kwa wakati na kuondoa unyanyapaa”amesema Said Makora mwakilishi kutoka Wizara ya Afya.
Akikumbusha kuhusu dalili za ugonjwa wa Marburg Dkt.Emmanuel Mnkeni kutoka Wizara ya Afya amesema dalili za ugonjwa huo zinaweza kuonekana kuanzia siku ya 2 hadi siku ya 21 ambazo zinaweza kufanana na magonjwa mengine kama vile Malaria, UTI, ambapo hupelekea homa, mwili kuishiwa nguvu,macho kuwa mekundu, vidonda vya koo, maumivu ya tumbo na dalili za baadae kutokwa damu sehemu za wazi za mwili.
Mratibu wa Tanzania Interfaith Partnership Livinus Ndibalema amesema kwa kushirikiana na Wizara ya Afya,Ofisi ya Rais TAMISEMI wameamua kutoa mafunzo ya ugonjwa wa Marburg kwa kundi muhimu la madiwani kwani wao wana ushawishi mkubwa kupeleka ujumbe katika jamii wanayoiongoza.
Katika mafunzo hayo Madiwani wameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na TIP kwa kuweza kudhibiti ugonjwa huo mpaka sasa hivyo wameahidi kuwa mabalozi huku Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba Godson Rwegasira kwa niaba ya madiwani akiiomba serikali kusitisha uvaaji wa kofia ngumu (Helment)kwa abiria katika kipindi hiki kwani inaweza kuwa chanzo cha maambukizi ya ugonjwa wa Marburg kupitia jasho.
Akijibu hoja hiyo,Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Gerald Manase amesema hoja hiyo ya Madiwani wataifanyia kazi .
Mafunzo hayo ya Waheshimiwa Madiwani ni mwendelezo wa uelimishaji wa Wizara ya Afya ,Ofisi ya Rais TAMISEMI ,Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kila kundi na jamii inafikiwa na elimu ya ugonjwa wa Marburg.