Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula amewaagiza Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za mitaa kupima, kulinda na kusimamia maeneo yote ya umma na maeneo ya wazi ili kuondokana na mwenendo mbaya unaoendelea kukithiri wa kuvamia maeneo hayo.
Agizo hilo amelitoa Machi 29 jijini Dodoma kwenye mkutano Mkuu wa Nane wa mwaka wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji ambapo alisema kumejitokeza utaratibu mbaya na usiovumilika, wa kuvamia maeneo ya wazi na ya umma pamoja na maeneo hatarishi na kuyabadilisha kuwa ya matumizi mengine hasa makazi.
Amesema Maeneo hatari kimazingira pamoja na maeneo ya wazi, yakiwemo maeneo maalum kwa matumizi ya baadaye (land bank), yanapaswa kupimwa na kulindwa dhidi ya wavamizi.
Alisema ili tuwe na miji nadhifu na iliyopangwa vyema katika nchi yetu hakuna budi kuanza kusimamia upangaji wa miji midogo na vitovu vya vijiji vyetu.
"Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi 2022 inaonyesha kuwa miji inakuwa kwa asilimia 4.8 na taarifa tulizonazo tuna jumla ya miji midogo inayochipukia 4,310 nchini ambayo isiposimamiwa ipasavyo itakuwa miji holela ya baadae," Alisema.
"Kwa kutambua umuhimu wa miji hiyo na uwepo wa kasi ndogo ya upangaji wa vijiji nchini, Wizara imeandaa mwongozo wa upangaji na ujenzi wa nyumba bora vijijini ili kuwezesha jamii yetu kuanza kupanga maeneo yao kuanzia vijijini," alisema Waziri Mabula.
Aidha alitoa maelekezo kwa Bodi na wanataaluma wote kuweka mkazo Zaidi katika namna ya kuzuia miji yetu midogo na vijiji kuwa makazi holela ya baadae kwa kusimamia na kuelimisha jamii matumizi ya mwongozo wa upangaji na ujenzi wa nyumba bora vijijini.
Pia alisema Serikali itaendelea na jukumu lake la kuimarisha mahusiano ya kitaasisi ili kuimarisha maendeleo ya miji pamoja na kupata fedha kwa ajili ya kupanga na kusimamia miji.
Hata hivyo aliekeza kuwa gharama za kuweza kumudu kupanga, kupima na kumilikisha maeneo yote nchini ni kubwa, Ninaelekeza Mamlaka za Upangaji nchini kutenga fedha kutokana na mapato ya ndani ya kila mwaka, kwa ajili ya kazi ya kupanga, kupima, kumilikisha, kuendeleza na kusimamia miji katika maeneo yao.