WAZIRI AWESO AHITIMISHA ZIARA YA KIKAZI MAREKANI.

MUUNGANO   MEDIA
0

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameshiriki kikao na kutoa shukrani na kuagana na watumishi wa uwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York. 

Watumishi hao wameongozwa na Mhe. Balozi Dkt. Suleiman Haji Suleiman, Kaimu Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Umoja wa Mataifa.

Mhe. Aweso amewashukuru kwa maandalizi na kufanikisha ushiriki wa Tanzania kwenye Mkutano wa Maji wa Umoja wa Mataifa uliofanyika tarehe 22 hadi 24 Machi 2023 katika ukumbi wa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Amesema kupitia usaidizi wa ubalozi wa Tanzania, nchi iliweza kuwasilisha hotuba ya Taifa kueleza namna Tanzania ilivyopiga hatua katika kuwapatia huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza wananchi wake pamoja na mipango mbalimbali iliyopo katika kuendeleza sekta ya maji kama sehemu ya utekelezaji wa Lengo namba 6 la Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.

Amemshukuru balozi na timu yake kwa kufanikisha kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kujadiliana namna wadau hao wanaweza kuisaidia Tanzania kutekeleza progamu yake ya maji ya mwaka 2023 - 2030 inayotarajiwa kuzinduliwa mwezi Mei 2023.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)