VIFO VITOKANAVYO NA UGONJWA WA KIFUA KIKUU VIMEPUNGUA KWA ASILIMIA 55.

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Na. WAF - Simiyu, Bariadi.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kasim Majaliwa amesema vifo vinavyosababishwa na Kifua Kikuu vimepungua kutoka vifo 55,000 vilivyotokea mwaka 2015 hadi vifo 25,800 sawa na asilimia 55% kwa Tanzania. 

Hayo ameyasema leo Machi 24, 2023 kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa mwaka 2022  kwenye Maadhimisho Siku ya Kifua Kikuu Duniani ambapo Kitaifa yamefanyika katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu. 

“Halikadhalika tumepunguza maambukizi mapya ya Kifua Kikuu kutoka kiwango cha wagonjwa 306 katika kila idadi ya watu 100,000 kufikia wagonjwa 208 katika kila watu 100,000 ikiwa ni sawa na punguzo la asilimia 32.” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amebainisha kuwa ugojwa wa Kifua Kikuu ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na vimelea aina ya bakteria ambao unaambukizwa kwa njia ya hewa kutoka kwa mgonjwa wa Kifua Kikuu ambaye hajaanza matibabu kwenda kwa mtu mwingine.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 duniani zenye maambukizi makubwa ya ugonjwa wa Kifua Kikuu ambazo kwa pamoja zinachangia asilimia 87 ya wagonjwa wote duniani.” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Pia, Waziri Mkuu amesema kuwa Pamoja na ukubwa huu wa tatizo hili, Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi na kuwekeza katika huduma za Kifua Kikuu ikiwemo kuongeza wigo wa huduma ili kuwafikia wananchi hususani katika maeneo yenye maambukizi makubwa ya ugonjwa huu hapa nchini. 

Hata hivyo, Wazri Mkuu Majaliwa amesema Ifahamike kuwa Kifua Kikuu ni ugonjwa mtambuka ambao sekta ya afya pekee haitoshi kutokomeza, hivyo ni budi kuweka mkakati wa kitaifa utakaowezesha  ushiriki wa sekta nyingine katika kutokomeza Kifua Kikuu ifikapo mwaka 2030.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)