Kilele cha Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kinatarajia kufanyika Aprili 13, 2023 Jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na waandishi mahiri kutoka nchi mbalimbali duniani.
Hayo yamesemwa leo Machi 29, 2023 kisiwani Zanzibar na Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari ambapo amesema tuzo hizo zitakuwa zikifanyika kila mwaka tarehe 13 Aprili ikiwa ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Waziri Mkenda ametaja malengo makuu ya tuzo hizo kuwa ni kukuza uandishi bunifu, kukuza usomaji, kuimarisha sekta ya uchapishaji na, kuhifadhi na kueneza utamaduni wa nchi yetu na kuongeza kuwa Serikali inatamani wapatikane waandishi mahiri wa Kitanzania ambao uandishi wao utashindanishwa katika tuzo za kimataifa.
"Tungependa huko mbele ya safari tuwe na waandishi bunifu wa Kitanzania ambao uandishi wao utakuwa maarufu sana duniani, watu watatafsiri vitabu vyao katika lugha mbalimbali ili nao waweze kushinda tuzo za kimataifa kama ya Nobel," ameongeza Prof. Mkenda.
Prof. Mkenda amesema tuzo hii itatolewa kwa wanaoandika kwa lugha ya Kiswahili na itakuwa inatolewa katika nyanja sita ambazo ni riwaya, hadithi fupifupi, mashairi, vitabu vya watoto, tamthilia na tafsiri ya vitabu vingine. Ameongeza kuwa kwa Mwaka huu tuzo zitatolewa katika uandishi wa Riwaya na Mashairi.
"Katika kila nyanja mshindi wa kwanza atapewa kitita cha Shilingi milioni 10, wa pili milioni 7 na wa tatu milioni 5. Wengine 7 wataungana na hawa watatu jumla 10, kila mmoja atapewa cheti cha kutambuliwa," amefafanua Waziri Mkenda.
Mhe. Ali Abdulgulam Hussein, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar akizungumza katika kikao hicho amesema mkutano na wanahabari umefanyika Zanzibar kwa kuwa tuzo hizo zinahusisha pande zote mbili za muungano.
"Mkutano huu kufanyika huku Zanzibar ni kuonesha kuwa hizi wizara zetu mbili zinafanya kazi kwa ushirikiano na hili suala linahusu waandishi bunifu kutoka pande zote mbili," amesema Mhe. Ali Hussein.