OR- TAMISEMI
Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( OR-TAMISEMI), Erick Kitali amewashukuru wadau wa maendeleo KOICA na PMC kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha usimamizi wa taarifa za utoaji wa huduma za afya kupitia mfumo wa usimamizi wa taarifa za vituo vya afya (GoT-HoMIS) katika Mkoa wa Dodoma.
Kitali amebainisha hayo Machi 23, 2023 katika kikao kazi cha Kamati ya Ushauri ya mradi wa upanuzi wa matumizi ya mfumo wa
GoT-HoMIS katika Mkoa wa Dodoma.
" Tuendelee kushirikiana kwa pamoja kutimiza malengo ya mradi na kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi" Ameeleza Kitali
Lengo la kikao hiko ni kupitia na kujadili utekelezaji wa mradi huo pamoja na kuweka mipango madhubuti ya utekelezaji wa mradi ili kuongeza wigo na kuboresha matumizi ya mfumo wa GOT-HOMIS katika vituo vya kutolea huduma za afya Mkoa wa Dodoma.
Mfumo wa GoT-HoMIS ambao kwa sasa unatumika kwenye vituo zaidi ya 1,400 nchi nzima, umelenga kuimarisha utoaji wa huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya, kutoa taarifa za magonjwa na wagonjwa kwa usahihi na wakati na kusimamia rasilimali fedha na dawa.
Kikao kazi hicho kimehusisha wataalam kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( OR-TAMISEMI), Wizara ya Afya, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, wadau wa maendeleo KOICA pamoja na PMC.