KAMATI YA LAAC YAPONGEZA UONGOZI NA WALIMU SHULE YA SEKONDARI LINDI.

MUUNGANO   MEDIA
0

 Na Asila Twaha, Lindi MC.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC) imewapongeza viongozi na walimu wa Shule ya Sekondari Lindi kwa kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwenye usimamizi wa rasilimali fedha na watu na kuifanya elimu kuwa bora na kuongeza ufaulu Mkoani Lindi.

Hayo ameyasemwa Machi 23, 2023 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa Mhe. Halima Mdee (Mb) wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Lindi Mkoani Lindi.

Amesema lengo la ziara katika shule hiyo ni kutaka kujua matumizi ya fedha zilivyotumika za ukarabati wa shule ambapo Serikali ilitoa fedha kwa ajili ya ukarabati.

“hii kamati ya LAAC inawakilisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni vizuri tujue fedha hizi zilizoletwa hapa zimetumikaje” amesisitiza Mhe. Mdee

 Awali akisoma taarifa Mkuu wa Shule ya Sekondari Lindi Bw. Ramadhani Divele ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha na kuweka mazingira mazuri katika sekta ya elimu ambapo zaidi ya shilingi milioni 725 na zilitolewa kwa ajili ya ukarabati wa shule hiyo.

Amefafanua kuwa fedha hizo zilifanya ukarabati wa vyumba vya madarasa 17, nyumba za walimu 7, mabweni 6, bwalo la chakula 1, matundu ya vyoo 37 maabara 3 na kuweka mifumo ya gesi na maji, jengo la utawala, jiko na stoo ya chakula.

Amesema fedha hizo za ukarabati zilitokana na programu ya EP4R lakini pia shule ilipokea tsh. milioni 10 kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi kwa ajili ya kulipia gharama za maji na mafundi waliokuwa wamekarabati nyumba sita za walimu.

Amesema uwepo wa mazingira rafiki ya kujifunzia na kufundishia imesaidia kupanda kwa taaluma lakini pia umoja na ushirikiano baina ya walimu kwa walimu, wanafunzi kwa walimu na wanafunzi kwa wanafunzi amewezesha kufanya vizuri kwenye mitihani ya kidato cha sita kwa miaka mitatu kutoka 2020-2022.

Aidha, amesema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,448 wasichana 460 na wavulana 988 na kwa upande wa kidato cha nne inafanya vizuri na kuendelea na jitihada kuhakikisha ufaulu unaongezeka na kufika asilimia 100.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)