ELIMU KUHUSU USHIRIKISHWAJI WA WATANZANIA KATIKA SEKTA YA MADINI YAENDELEA KUZAA MATUNDA

MUUNGANO   MEDIA
0

 Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini wa Tume ya Madini, Venance Kasiki amesema kuwa tangu kuanza kwa awamu ya kwanza ya utoaji wa elimu kuhusu ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini kupitia mikutano na majukwaa mbalimbali, matokeo makubwa yameonekana ikiwa ni pamoja na kampuni nyingi zinazomilikiwa na watanzania kujiingiza kwenye utoaji wa huduma na bidhaa kwenye migodi ya madini ikiwa ni pamoja na vifaa vya uchimbaji, ulinzi na vyakula.

Kasiki ameyasema hayo leo Machi 24, 2023 kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba kwenye kikao na kampuni ya Rock Solution Limited kilichofanyika kwenye ofisi za makao makuu ya Tume ya Madini jijini Dodoma kwa ajili ya kampuni hiyo kutambulisha huduma zake ikiwa ni pamoja na mpya ya utengenezaji wa makasha ya kubeba sampuli za madini kwenye migodi ya madini.

Kikao hicho pia kimeshirikisha watendaji kutoka Tume ya Madini Makao Makuu na wataalam kutoka katika Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), Mgodi wa Dhahabu wa Shanta, Tembo Nickel, Noble Helium, Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu, Kampuni ya Uchimbaji wa Madini ya Kinywe ya Lindi Jumbo, Rubalis Resources, Kampuni ya Uchorongaji ya Amazon na  Benki ya CRDB.

Amesema kuwa, Tume ya Madini kupitia Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya Madini imekuwa ikitoa elimu katika maeneo mbalimbali nchini kuhusu ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini, kupitia maonesho, makongamano na majukwaa na kusisitiza kuwa hivi karibuni lilifanyika Jukwaa la Pili la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini lililoambatana na maonesho lililofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 15 hadi 17 mwezi Machi mwaka huu.

Ameendelea kusema kuwa hatua ya sasa inayofanyika ni kufanya uhamasishaji kwa kampuni za kitanzania kuanza kuzalisha bidhaa bora zitakazotumika kwenye migodi ya madini na kujipatia faida huku Serikali ikipata kodi mbalimbali na kuongeza ushirikishwaji wa Watanzania kwenye Sekta.

Akielezea manufaa ya uwekezaji wa watanzania katika uzalishaji wa bidhaa na huduma kwenye migodi ya madini, Kasiki amesema kuwa ni pamoja na kuzalisha ajira, huduma na bidhaa kupatikana kwa gharama nafuu na Serikali kuendelea kupata mapato kupitia kodi mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Kasiki amesema kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto za wasambazaji wa bidhaa na huduma kwenye migodi ya madini na kusisitiza kuwa milango ipo wazi kwa watanzania wenye nia ya kuwekeza kwenye Sekta ya Madini ambapo ofisi ipo tayari kutoa elimu na kutoa msaada.

Aidha amezitaka Taasisi za kifedha kuendelea kuwakopesha watanzania wenye nia ya kujihusisha na shughuli za uchimbaji wa madini na utoaji wa huduma na bidhaa kwenye migodi ya madini ili kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na kuzalisha ajira nyingi zaidi.

Wakati huohuo akizungumza kwenye kikao hicho, Mkurugenzi wa kampuni ya Rock Solution Limited, Zacharia Nzuki ameipongeza Tume ya Madini kwa usimamizi mzuri wa kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini zilizotengenezwa mwaka 2018 ikiwa ni sehemu ya maboresho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 yaliyofanywa  mwaka 2017.

“Tume ya Madini imekuwa ni msaada mkubwa sana kwa kampuni za kitanzania zinazotoa huduma na bidhaa kwenye migodi ya madini kupitia usimamizi makini wa utekelezaji wa kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini, kabla ya maboresho ya kanuni hizo kampuni nyingi za madini zilikuwa zikiagiza bidhaa kutoka nje ya nchi,” amesema Nzuki.

Awali akielezea kampuni hiyo, Mtaalam wa Biashara kutoka Rock Solution  Erasmo Haule amesema kampuni hiyo iliyoanzishwa mapema mwaka 2015 inamilikiwa na watanzania kwa asilimia 100 ambapo inatoa huduma ya vifaa mbalimbali kwenye kwenye migodi ya madini.

Ameongeza kuwa kampuni hiyo inatarajia kujenga kiwanda mkoani Mwanza kwa ajili ya kutengeneza makasha ya kubeba sampuli za madini kwenye migodi ya madini ambapo uzalishaji wake unatarajiwa kuanza mwezi Oktoba 2023 na kuanza na kutoa ajira 150

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)