Mkuu wa Wilaya ya Wanging'ombe Mhe. Claudia Kitta amezindua rasmi zoezi la uwekaji vigingi katika Wilaya ya Wanging'ombe lengo likiwa ni kutenganisha eneo la Pori la Akiba Mpanga/Kipengere na ardhi ya vijiji.
Akizungumza wakati wa zoezi la uwekaji vigingi lililozinduliwa Machi 27, 2023 wilayani humo, Mhe. Claudia amewataka wananchi Wote kushiriki kikamilifu katika zoezi la uwekaji vigingi na kutahadhalisha kuwa hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa Kwa yeyote atakayehusika katika kukwamisha zoezi hilo.
Mkuu huyo wa Wilaya, amewaagiza wakazi wa kitongoji cha Soliwaya ambao baadhi ya kaya zake zitakuwa ndani ya mpaka mpya wa Hifadhi kutoendeleza shughuli za kibinadamu ikiwa ni pamoja na kujenga makazi mapya kwani Serikali inaendelea na uthaminishaji wa maendelezo waliyoyafanya Ili waweze kulipwa na baadae kuhamishiwa kwenye eneo lililopunguzwa kutoka kwenye ardhi ya Hifadhi na kuwa ardhi ya Kijiji.
Aidha, Mhe. Claudia amewataka wananchi Wote kuheshimu sheria za Uhifadhi na wajitahidi kutunza mazingira ya Hifadhi na mazingira katika makazi yao Kwa ujumla.
Hizi ni jitihada za dhati za Serikali kuhakikisha inatatua mgogoro wa matumizi ya ardhi baina ya Pori la Akiba Mpanga/Kipengere na Vijiji vya Igando, Mpanga Mpya, Luguda, Hanjawanu, Imalilo, Wangama na Wangamiko uliodumu Kwa muda Mrefu wilayani Wanging'ombe.