WATUMISHI TFRA WATAKIWA KUDUMISHA MSHIKAMANO, WAPONGEZWA KWA KUJITUMA.

MUUNGANO   MEDIA
0

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania(TFRA), Dkt. Stephan Ngailo amewataka watumishi wa mamlaka hiyo kufanya kazi kwa weledi na kujituma huku wakiimarisha Amani, mshikamano, umoja na upendo miongoni mwao.

Amesema, kuimarisha hayo kutaongeza manufaa katika utendaji mzuri na wa kujituma kwa mtu mmoja mmoja na mamlaka kwa ujumla kuliko kuendekeza malumbano na migongano ambayo haina tija miongoni mwao.

Dkt. Ngailo ameyasema hayo, tarehe 17 Februari, 2023 alipokuwa akizungumza na menejimenti ya mamlaka na wawakilishi wa watumishi walioshiriki kikao cha Baraza la wafanyakazi wa mamlaka hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa St. Gasper Jijini Dodoma.


Ameongeza kuwa, katika maisha na utendaji wa kila siku kila mmoja ana utu wake na hivyo anastahili kuheshimiwa jinsi alivyo, na kuongeza kuwa utendaji wetu unategemeana kuanzia mtu wa ngazi ya chini kabisa mpaka kwa yule wa ngazi ya juu.

“ Sisi sote tunategemeana, tudumishe umoja mahala pa kazi” alisisitiza Dkt. Ngailo.

“ Tusiwe na migongano migongano, tuwe na lugha za staha miongoni mwetu, tujengane ili kila mmoja afanikiwe katika kazi zake” Dkt Ngailo alikazia.

Aidha, Dkt. Ngailo alimtaka Meneja wa Kitengo cha ukaguzi wa ndani wa Mamlaka kutoa mafunzo kwa watumishi wa mamlaka juu ya majukumu ya kitengo hicho pamoja na kuwajengea uwezo wa kuheshimu sheria na taratibu zinazosimamia mamlaka hiyo na hivyo kuwawezesha kuepusha hoja mbalimbali za kiutendaji miongoni mwao.

Akiwasilisha mada juu ya utendaji wa kitengo cha ukaguzi wa ndani Kaimu Meneja wa kitengo hicho, Pauline Mganga amesema, uwepo wa kitengo hicho si kutoa hoja za kiukaguzi bali ni katika kuimarisha udhibiti wa ndani, usimamizi wa vihatarishi na utawala bora wa mamlaka pamoja na kutoa uhakikisho unaohitajika kuhusu ufanisi wa mfumo wa udhibiti wa ndani, usimamizi wa vihatarishi na taratibu za utawala.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa huduma za mamlaka, Bi. Victoria Elangwa aliwapongeza wajumbe wote walioshiriki kikao hicho na kuwataka kwenda kuwaeleza watumishi wengine wanaowawakilisha kutoka idara na vitengo vya mamlaka ili wawe na uelewa wa mambo mema yaliyojadiliwa katika kikao hicho.

Aidha, amewasihi viongozi na watumishi kuwasilisha taarifa mbalimbali za robo, nusu na mwaka za utekelezaji wa majukumu ili zifikishwe zinakohusika kwa wakati na kuepusha utendaji mbovu kwa kutii mamlaka na taratibu za kiutumishi.

Naye Mwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi TUGHE Makao Makuu, Deus Kaetano amepongeza namna kikao cha baraza kilivyoendeshwa na kuwasihi watumishi kuwasilisha hoja zilizojadiliwa kwa watumishi waliobaki makao makuu jinsi zilivyo.

Pia ameshauri watumishi wa mamlaka kujiunga na chama hicho ili kuweza kunufaika na masuala mengine mazuri yanayotekelezwa na chama hicho kwa wanachama wake.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)