VIONGOZI MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA WATAKIWA KUTATUA CHANGAMOTO ZINAZOKWAMISHA WANANCHI KUPATA HUDUMA BORA

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika halmashauri kutatua changamoto zinazokwamisha wananchi kupata huduma bora pindi wanapofuata huduma katika maeneo yao ya kazi.

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo jijini Dodoma, wakati akifunga kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kilichofanyika kwa siku tatu katika ukumbi wa Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali Mtumba.

Mhe. Ndejembi amesema, viongozi hao wanapaswa kukerwa na changamoto zinazowakabili wananchi pindi wanapofuata huduma katika maeneo yao ya kazi na kuchukua hatua stahiki ya kuwahimiza watendaji wanaowasimamia kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi.

Mhe. Ndejembi amewahimiza viongozi hao, ambao wengi wao wanatoka maeneo ya pembezoni kuhakikisha wanasimamia vema rasilimaliwatu ili wananchi wapate huduma bora, kwani wananchi wengi waishio pembezoni mwa nchi wanalazimika kutumia gharama kubwa kufuata huduma kwenye ofisi za makao makuu ya mikoa na halmashauri za wilaya.

Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka viongozi hao kutatua changamoto zinazowakabili watumishi ili wasiwe na sababu ya kutotoa huduma bora kwa wananchi na kuongeza kuwa, anaamini viongozi hao wanatambua wajibu wao katika kutatua kero za watumishi na wananchi kwa ujumla. 

“Kuna changamoto ambazo mnahitaji kuwasikiliza tu watumishi au wananchi na kutoa majibu sahihi, lakini mmekuwa na tabia ya kukwepa jukumu hilo na kulielekeza kwa Katibu Mkuu-UTUMISHI jambo ambalo si sahihi kwani lipo ndani ya mamlaka zenu na uwezo wenu kiutendaji,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu wa Halmashauri ya Mji Handeni, Bw. Steven Bavu amesema watahakikisha wanatekeleza agizo la Mhe. Ndejembi la kutatua kero za wananchi katika maeneo yao ya kazi.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)