Na.Elimu ya Afya kwa Umma.
Kutokana na serikali kuongeza kasi ya elimu na uhamasishaji umuhimu wa chanjo ya Surua katika mkoa wa Katavi hasa kwa kuanzisha kampeni ya chanjo ya nyumba kwa nyumba na kwenye mikusanyiko ya watu, mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Magdalena Kulwa mkazi kijiji cha Mwamabambasi kata ya Chamalendi Halmashuri Mpimbwe Wilayani Mlele Mkoani Katavi ameitikia hamasa hiyo baada ya kuleta watoto saba wa familia moja kupata chanjo hiyo.
Akizungumza katika kijiji hicho baada ya timu ya watalaam kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na halmashauri ya Mpimbwe kufika katika kijiji hicho kutoa elimu Magdalena amesema ugonjwa wa Surua sio wa kufanyia mzaha ndio maana wao kama familia wameamua kuwakusanya watoto wote 7 wa familia moja wakiwemo watoto watoto wake wawili kupata chanjo kwani kuanzia sasa wameujua ukweli baada ya kusikia kampeni ya Chanjo kupitia matangazo ya kwenye magari.
“Nawaambia na wengine wawalete wapate chanjo wasiwapeleke kwa Waganga wa Tiba Asili,nimetoka kazini nimewaleta kuna ugonjwa mkali sasa hivi, ugonjwa huu sio wa kuwapeleka kwa Waganga”amesisitiza Magdalena.
Ikumbukwe kuwa serikali kupitia wizara ya afya imeongeza msukumo wa utoaji wa elimu na uhamasishaji wa chanjo ya Surua katika mkoa wa Katavi kwa kutoa magari ya matangazo kwa ajili ya uhamasishaji ambapo hamasa imeshaanza kuzaa matunda baada ya wananchi kuanza kujitokeza kuwapatia watoto chanjo huku wakiiomba serikali kuongeza chanjo.