JAMII ISHIRIKIANE NA WALIMU KUINUA TAALUMA

0

 

Mmoja wa wakufunzi akiendesha mjadala kuhusu namna bora ya kufundisha KKK kwa wanafunzi wa elimu ya awali kwenye mafunzo ya ujifunzaji na ufundishaji walimu wa madarasa ya awali, la kwanza na la pili yanayoendelea wilayani Nkasi na kuratibiwa na Taasisi ya Elimu Tanzania na pamoja na Programu ya Shule Bora.



 Sehemu ya walimu wakuu, walimu wa taaluma , waelimisha rika na maafisa elimu kata toka shule 40 za mkoa wa Rukwa wakendelea na mafunzo kuhusu mbinu za kufundisha KKK inayoratibiwa na Taasisi ya Elimu Tanzania.



Waratibu wa mafunzo kwa walimu na maafisa elimu kuhusu namna ya kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa KKK kwa madarasa ya  awali, la kwanza na la pili wakifuatilia majadiliano na wadau jana mjini Namanyere.


Mkufunzi Rose Chipindula toka Taasisi ya Elimu Tanzania akifundisha namna  bora ya ufundishaji irabu kwa wanafunzi wa madarasa ya awali,la kwanza na la pili kwenye mafunzo ya  walimu wakuu, walimu wa taaluma, waelimisha rika na maafisa elimu kata yaliyofanyika Februari 14,2023 wilayani Nkasi ambapo jumla ya walimu 140 toka shule 40 walishiriki.


Mawasilisho ya mada zinazofundishwa kuhusu namna bora ya ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi wa elimu ya awali, darasa la kwanza na la pili kwenye mafunzo ya walimu toka shule 40 za mkoa wa Rukwa yanaratibiwa na Taasisi ya Elimu Tanzania.

(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa).


Na OMM Rukwa

 Jamii imetakiwa kutoa ushirikiano kwa walimu ili kuleta ufanisi utakaochangia  kuboresha taaluma ya wanafunzi  wa madarasa ya awali na la kwanza kwenye shule za msingi za umma .


Kauli  mbalimbali zimetolewa Februari 14,2023  na walimu wanaoshiriki mafunzo ya kuwajengea uwezo na mbinu za ujifunzaji na ufundishaji KKK yanayotolewa  na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia  kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania wilayani Nkasi.


Shule Bora ni programu ya serikali inayolenga  kuinua ubora wa elimu jumuishi,mazingira salama ya kujifunzia kwa wasichana na wavulana kwenye shule za umma nchini Tanzania na inafadhiliwa na Shirika la Misaada la Uingereza (UKaid) kutoka Serikali ya Uingereza.


Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kirando iliyopo Nkasi Gerald Kossamu amesema wazazi na serikali wanatakiwa kuungana kuondoa tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa na upungufu wa walimu unaoathiri ufundishaji.


Kossamu alisema shule yake ina changamoto ya wingi wa wanafunzi ambapo hadi kufikia (jana ) Februari  13 mwaka  huu shule imeandikisha jumla ya wanafunzi wa elimu ya awali 443 na wanafunzi 601 wa darasa la kwanza.


“Msongamano ni mkubwa madarasani ambapo shule ina wanafunzi 3,174 na walimu 23 ambao hawatoshi . Walimu inawawia ugumu katika ufundishaji hata namna ya kudhibiti utoro.Serikali itusaidie madarasa ya kutosha” alisema Mwalimu Kossamu.


Happiness Aristides ni mwalimu wa taaluma toka shule ya msingi Mteta iliyopo Laela, halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga alisema wazazi na walezi washirikishwe ili waweze kudhibiti utoro wa watoto unaochangia kufeli masomo.


Happiness aliongeza kusema watoto wanastahili kupendwa na kusaidiwa ili wa waone umuhimu wa kujifunza na kuzingatia masomo hususan walio madarasa ya awali na darasa la kwanza ndio maana mafunzo kwa walimu ni muhimu.


Kuhusu manufaa ya mafunzo ya programu ya Shule Bora ,mwalimu Happiness alisema yamemsaidia kujiamini kwa kupata mbinu stahiki za kufundisha madarasa ya awali .


Kwa upande wake Mratibu wa Programu ya Shule Bora Tanzania  toka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Mwesiga  Kabigumila alisema lengo la mafunzo kwa viongozi hao wa walimu ni kuwajengea mbinu na uwezo wa kumudu na kutambua  tabia za wanafunzi na jinsi ya kuwahudumia.


Mwesiga aliongeza kusema kumekuwepo na tatizo la utolewaji wa taarifa zisizo za uhakika au uhalisia toka kwa walimu na baadhi ya  wasimamizi wa elimu hatua inayopoelekea serikali au mradi kushindwa kutambua shida za watoto kutomudu KKK.


“Ni bora walimu wakuu, wasimamizi wa shule na maafisa elimu   kujikita katika utoaji taarifa sahihi ili kusaidia taifa na mradi wa Shule Bora kuweka mikakati ya   suala  la ujifunzaji na ufundishaji KKK” alisisitiza Mwesiga.

Programu ya Shule Bora imeendesha mafunzo ya uboreshaji wa ufundishaji na ujifunzaji wa darasa la awali, la kwanza na la pili ambapo leo ilikuwa zamu ya kundi la pili  walimu wakuu, walimu wa taaluma, waratibu elimu kata na waelimisha rika toka shule arobaini (40) za msingi za mkoa wa Rukwa.

Mwisho.


Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)