IRUWASA YAVUKA LENGO LA CHAMA TAWALA LA KUSAMBAZA HUDUMA YA MAJI IRINGA.

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Na Gideon Gregory, Dodoma.

Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira mkoani Iringa (IRUWASA), imefanikiwa kuvuka lengo la sera ya Maji na Ilani ya Chama tawala ya kutoa huduma ya usambazaji maji kwa mji wa Iringa na maeneo ya pembezoni kwa 97% kwa wakazi wa mjini na 95% Vijijini huku huduma hiyo ikipatikana kwa masaa 23 kwa siku.

Mafanikio hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa IRUWASA Mhandisi David Pallangyo leo Februari 27,2023 Jijini Dodoma mbele ya waandishi wa habari wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo na kusema kuwa wamekuwa mamlaka chache nchini zinazotoa huduma hiyo kwa muda mrefu zaidi.

“Mafanikio haya ya kupatikana kwa huduma ya maji masaa 23 kwa siku yamefikiwa ndani ya miaka mitatu mpaka minne,”amesema Pallangyo.

Pallangyo ameongeza kuwa Serikali imepanga kutekelza mradi mkubwa wa uboreshaji wa huduma za majisafi na uondoshaji wa majitaka katika Manispaa ya Iringa, Miji ya Kilolo na Ilula pamoja na baadhi ya vijiji vilivyo kandokando ya njia ya bomba kuu la maji kutoka Kilolo hadi Mjini Iringa. 

Amesema mradi huo utatekelezwa na Serikali ya Tanzania kupitia mkopo wenye masharti nafuu kutoka Serikali ya Korea wenye thamani ya dola za Marekani milioni 88.4. 

“Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi Mei 2023 kwa Mhandisi Mshauri (Consultant) kufanya upembuzi yakinifu wa kina (detailed design) na ujenzi unatarajiwa kuanza mwezi Aprili 2024 na kukamilika mwaka 2027,”amesema.

Aidha ameongeza kuwa pamoja na mafanikio iliyoyapata, IRUWASA bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo suala la uchafuzi na Uharibifu wa Vyanzo vya Maji huku shughuli za kibinadamu wanazofanyia katika vyanzo vya maji kama vile kilimo, ufyatuaji wa matofali, mifugo, ukataji miti, uchimbaji wa mchanga/mawe vimekuwa changamoto kubwa kwani vimekuwa vikipelekea kupungua kwa kina cha mto Ruaha mdogo hasa wakati wa kipindi cha kiangazi.

“Kikosi kazi kimeundwa kikishirikisha wajumbe kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na Ofisi ya Bodi ya Maji Bonde la Rufiji kwa ajili ya kusimamia shughuli za utunzaji wa vyanzo vya maji, kikosi kazi hiki, kinatoa elimu juu ya umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji, kinasimamia shughuli za kupanda miti rafiki wa mazingira, kufuga nyuki na kusimamia utekelezaji wa sheria za mazingira,”ameongeza.

Ikumbukwe kuwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Iringa (IRUWASA) ilianzishwa Julai Mosi mwaka 1998 kwa mujibu wa Sheria ya Maji Na. 8 ya mwaka 1997 ambayo ilifanyiwa mabadiliko na Sheria ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Na 12 ya Mwaka 2009 na baadae Sheria Na. 5 ya Mwaka 2019. 

Ambapo ilianzishwa ikiwa daraja C ikitegemea ruzuku ya Serikali (Wizara ya Maji) katika uendeshaji, hata hivyo, ilipanda kutoka daraja C hadi B mnamo mwaka 2003 na baadaye daraja A mwaka 2007 hivyo kujitegemea kwa 100% katika gharama za matengenezo na uendeshaji na sehemu ya uwekezaji.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)