Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akikagua maendeleo ya ujenzi
wa Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato ambao ujenzi wake umefikia asilimia
11.7 na utakapokamilika utaruhusu ndege 13 kutua kwa wakati mmoja na utahudumia
abiria Milioni 1.5 kwa kutumia mageti 8. Mhe. Senyamule amemtaka Mkandarasi wa
ujenzi kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametoa rai kwa wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa miradi ya kimkakati katika jiji la Dodoma kuzingatia ubora na viwango katika kukamilisha miradi kwa wakati.
Mhe.
Senyamule ameyasema hayo leo Februari 15, 2023 wakati wa ziara ya kikazi ya
kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Uwanja wa
Ndege wa kimataifa wa Msalato, barabara ya mzunguko LOT 1 inayotoka
Nala-Veyula-Mtumba-Ihumwa yenye urefu wa kilometa 52.3 na LOT 2 yenye urefu wa
Kilometa 60 inayotoka Dry pot Ihumwa, Ngo’ngo’na, Matumbulu, Bihawana – Nala.
“Mradi huu ni wa aina yake barani Afrika tunampongeza sana Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za kukamilisha ujenzi
wa kilometa 112.3 km za barabara za mzunguko ndani ya Mkoa wa Dodoma” Amefafanua
Mhe. Senyamule.
“Sisi
tunataka miradi yetu ikamilike ndani ya muda, sote tunafahamu miradi hii muhimu
inatakiwa kukamilika 2024 au mapema 2025 kama mkataba unavyoonyesha. Dhamira ya
serikali ni kusogeza huduma kwa wananchi na kuhikisha utekelezaji wa miradi hii
unanufaisha wananchi ikiwa ni pamoja na kuzingatia utoaji wa huduma kwa jamii (CSR)
kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na miongozo iliyopo. Hatutamani sana tunaanza
vizuri tunafika mahali tunaanza kutoa sababu nyingi, changamoto zitatueni
lakini zisipelekee kuongeza muda wa mradi kukamilika’’ Alisisitiza Mhe
Senyamule.
Akiwa
katika eneo la ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato unaojengwa na Mkandarasi
kutoka China Mhe Senyamule amemtaka
Mkandarasi huyo kuongeza kasi ya ujenzi wa jengo la abira ili liweze kukamilika
kwa wakati na kwenda sambamba na ujenzi wa njia za kuruka na kutua ndege.
“Hii miradi inabidi iende sambamba, hatuwezi kukamilisha mradi mmoja
nakuanza kuutumia maana yote inategemeana, hakuna mkwamo wowote fedha za ujenzi
zipo, sisi tunahakikisha kazi inaendana na kasi, lazima wakandarasi wajue
matamanio ya Serikali, fanyeni kazi usiku na mchana” Amesisitiza Mhe.
Senyamule.
Mradi
wa Ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato Lot 1
sehemu ya kwanza utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 165 na Lot 1 sehemu
ya 2 utagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 199
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri ametoa rai kwa Mkandarasi
huyo kuhakikisha anazingatia Mpango wa Usimamizi wa Mazingira ili miundombinu
inayojengwa hususan madaraja yaweze kupitisha maji kikamilifu bila kuathiri
wananchi na mazingira kwa upande wa pili.
Katika ziara ya siku moja ya kutembelea miradi ya kimkakati ndani ya Mkoa wa Dodoma, Mhe. Mkuu wa Mkoa alimbatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya.