WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Mji na
Wilaya za Mbinga wahakikishe kuwa wanaunda kanda za kilimo na
kuwasambaza maafisa kilimo wao badala ya kuwaacha wakae maofisini.
Ametoa
agizo hilo Ijumaa, Januari 5, 2018 wakati akizungumza na watumishi na
madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga pamoja na Halmashauri ya Mji
wa Mbinga, kwenye ukumbi wa Jumba la Maendeleo, mjini Mbinga.
“Mkurugenzi
wa TC na DC chuja maafisa kilimo ulionao na uhakikishe wanabakia watatu
tu. Abaki DALDO, mtu wa horticulture na mthamini, wengine wote
wasambaze kwenye kanda ili wasimamie wakulima wakiwa huko huko. Hili
litekelezwe na Mkuu wa Wilaya ulisimamie” alisema.
Aliwataka
maafisa kilimo wa zao la kahawa waende vijijini na kufanya sensa ili
waweze kubaini wana wakulima wangapi wanaozalisha kahawa. “Afisa kilimo
wa wilaya lazima ujue kijiji kina wakulima wangapi wa kahawa, na wana
ekari ngapi? Na katika ekari hizo, ana miche mingapi? Hii itaisaidia
Serikali ijue inahitaji dawa za aina gani, mbolea kiasi gani na miche
mingapi kwa wakulima wake,” alisema.
“Ninataka hizi takwimu ziwe zimekamilika ifikapo tarehe 28 Februari, mwaka huu,” alisisitiza.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka maafisa ushirika wa wilaya hiyo
wakasimamie uundwaji wa AMCOS mpya na kuimarisha zile za zamani ambazo
zinafanya kazi vizuri.
“Maafisa
ushirika ninataka nipate takwimu ya AMCOS very strong (ambazo ziko
imara) kwenye wilaya yako. Iifikapo tarehe 28 Febriari, takwimu hizi
ziwe zimekamilika. Kama kuna AMCOS nzuri ziimarisheni, itisha uchaguzi
ili uanze na uongozi mpya,” alisisitiza.
Aliwaeleza
watumishi na madiwani kwamba Serikali ya awamu ya tano imedhamiria
kurudisha heshima ya zao hilo ambapo zamani iliweza kusomesha watoto
kadhaa kwenda sekondari kutokana na mfuko wa kahawa.
“Zamani
zao la kahawa lilikuwa likisomesha watoto wa wakulima, sasa hivi hakuna
hata anayefaidika na zao hili. Tunataka zao hili liwanufainishe
wakulima, iinue uchumi wa wanaMbinga, isomeshe watoto na iwezeshe
wakulima kujenga majumba,” alisema.
Alisema
kuanzia msimu ujao wa Mei, Juni na Julai 2018, ununuzi wa kahawa
utafanywa na vyama vya msingi vinavyotambulika kwa maafisa ushirika.
Aliwaonya
watumishi wa Halmashauri hizo waache kutoa vibali vya ununuzi wa kahawa
kwa watu binafsi wanaomiliki kampuni za kununua kahawa. “Halmashauri
ndiyo mnatoa vibali vya kampuni kununua kahawa. Huu ni mwisho sasa.
Hatuna mnunuzi binafsi wala hatuna kampuni binafsi, hawa wote tukutane
kwenye mnada,” alisema.
Alisema
hataki kuona watumishi wa Halmashauri wakionesha vibali vya kununua
kahawa kama moja ya chanzo cha mapato kwenye Halmashauri hizo. “Ni
marufuku kuingiza vibali kwenye mapato ya Halmashauri,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,