Na Avelina Musa - DODOMA
MKURUGEZI Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma Mhe.Albina Mtambuka ameipongeza Shirika la Save the Children kwa kuendelea kuziunga Mkono juhudi za Serikali katika kutokomeza Utapiamlo katika jamii kwa kutoa elimu ya lishe na kugawa mbuzi wa maziwa.
Mhe.Albina amesema hayo wakati wa mahojiano maalum ambapo amesema Shirika la save the Children wamekuwa wadau muhimu na wa kuigwa kwa namna wanavyoiunga mkono serikali kupitia mradi wao wa Lishe yangu,Maisha yangu ambao unalenga kuboresha lishe kwa wamama na watoto chini ya miaka 5 pamoja na kuongeza kipato cha kaya maskini.
Albina amesema Wilaya ya Bahi walianza kwa kupata mbuzi 575 katika vijiji vyote 59 lakini mpaka sasa wamefikia mbuzi 1081 ambapo mradi umesaidia kuboresha lishe ya watoto chini ya miaka mitano na wamama kwa kuwapatia mbuzi hao wa maziwa pamoja na kuongeza kipato Cha familia.
"Wadau wetu walianza kutoa mbuzi 6 Kwa Kila Kijiji ambapo vijiji vyote 59 vilifikiwa na jamii zimepata faida kubwa kwa kuwapatia lishe Bora kupitia maziwa ,kipato na kuwawezesha kupata mbolea zinazoongeza tija katika shunghuli zao za kilimo cha bustani na mazao"amesema Albina.
Mhe.Albina ameiomba shirika kuendeleza mradi wa lishe yangu,Maisha yangu pamoja na kupeleka miradi mingine katika Wilaya ya Bahi ili kuendelea kuungana na serikali katika mapambano ya kutokomeza utapiamlo katika jamii.
Emanuel Meda ni mlengwa na mnufaika,Mkazi wa Asanje Kata ya Babayu Wilayani Bahi amesema amenufaika na mradi kupitia mbuzi aliyopata yeye kama baba wa watoto wa wawili ambapo lishe imeboreshwa zaidi tofauti na mwanzo na wanapata mbolea na anatarajia kupata mavuno mengi.
"Mimi kama baba wa familia niliupokea mradi huu kwa moyo wote ambapo umeleta manufaa makubwa katika familia yangu maana kwa sasa watoto wangu na familia kwa ujumla wanapata lishe Bora sana tofauti na mwanzo"amesema Emmanuel.
Aidha,David Msimbi ni Daktari wa mifugo Wilaya ya Chamwino amesema mradi wa Lishe yangu,Maisha yangu ulianza kutekelezwa mwaka 2023 katika wilaya hiyo wenye lengo la kuinua lishe katika kaya maskini hasa Kwa wamama na watoto chini ya miaka mitano.
Amesema katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino vijiji vyote 107 vilifikiwa na mradi wa Lishe yangu,Maisha yangu na kugawa mbuzi wa maziwa kwa walengwa waliokusudiwa.
"Lishe imeboreshwa na watoto wanaendelea vizuri tofauti na mwanzo ambapo jamii zetu zilikuwa hazizingatii ubora wa lishe lakin Kwa sasa wamepata elimu ya lishe Bora"amesema Dkt.Msimbi.
Kwa Upande wake,Mhudumu wa Afya ngazi ya Jamii kutoka Dabalo Wilaya ya Chamwino Erica Kaulule amesema mradi huo umesaidia kuondoa utapiamlo katika jamii tofauti na mwanzo ambapo hali ilikuwa mbaya katika maeneo ya vijijini familia nyingi hazikuwa na elimu ya lishe Bora.
"Kuna mtoto alikuwa na utapiamlo mkali sana lakini baada ya kumwingiza kwenye mradi huu alipata lishe Bora na sasa anaendelea vizuri tofauti na mwanzo"amesema Erica.






